Watu wengi wanaamini kutengeneza pesa nyingi zaidi kutatatua matatizo yao yote ya pesa. Ila mara nyingi husababisha matatizo makubwa zaidi. Moja ya sababu kubwa inayosababisha matatizo mengi ya pesa kwa watu ni kwamba hawajawahi kufundishwa jinsi ya kudhibiti mzunguko wao wa pesa. Wamefundishwa kujua kusoma, kuandika, kuendesha gari nk lakini sio namna ya kudhibiti mzunguko wao wa pesa. Bila ya kulijua hili wanaishia kuwa na matatizo ya pesa kila kukicha na kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi wakiamini kwamba kutengeneza pesa nyingi zaidi kutamaliza matatizo yao. JUA KWAMBA PESA NYINGI HAZITAMALIZA MATATIZO YAKO YA PESA KAMA UKISHINDWA KUDHIBITI MZUNGUKO WAKO WA PESA. Pesa nyingi zaidi huwafanya watu wengi kuwa maskini kwa sababu huongeza matumizi na kuangukia kwenye madeni makubwa kila mara wanapoongezwa mshahara.
Unatakiwa ukae chini uweke mpango wa kudhibiti matumizi na kupunguza madeni hali kadhalika kupunguza vitu ambavyo vinakupunguzia pesa mfukoni. Nimekuandalia hapa chini namna ambayo itakuwezesha kudhibiti mzunguko wako wa pesa.
Ila fanya hivi kabla sijakuambia:
(1) Ainisha kipato chako na matumizi yako kwa mwezi.
(2) Angalia eneo ambalo unazalisha kipato chako (mwajiriwa, umejiajiri, mmiliki wa biashara au mwekezaji)------Kumbuka mmiliki wa biashara ni yule ambaye anaweza akaondoka mbali na biashara yake hata mwaka au miaka miwili lakini akakuta biashara yake bado ipo au imekuwa zaidi. Ukiona huwezi kufanya hivyo basi jua umejipa kazi mwenyewe/ umejiajiri
(3) Ainisha eneo gani ambalo unataka kuzalisha pesa nyingi zaid baada ya miaka mitano (Baada ya miaka mitano unataka kuzalisha pesa nyingi kama mwajiriwa, aliyejiajiajiri, mmiliki wa biashara au mwekezaji?)
Haya sasa baada ya kufanya hivyo uko tayari kuanza mpango mkakati wa kudhibiti mzunguko wa pesa. Ni hatua mbili tu za kuzifanya:
(1) Jilipe mwenyewe kwanza
Tenga asilimia fulani kila unapopata kipato au mshahara wako kwa ajili ya kuwekeza. Na ukikitunza usikitoe ulipokitunza mf. Benki mpaka pale utakapoona kuwa uko tayari kuwekeza.
(2) Lipa deni
Kama una madeni basi tenga asilimia nyingine kwa ajili ya kulipa deni mpaka libakie sifuri na uongeze hiyo asilimia uliyoweka kulipa deni lako la mwisho kwa ajili ya kuwekeza. Na hakikisha kipindi unalipa deni usiongeze deni lingine.

No comments:
Post a Comment