Kuwekeza ni sehemu ambayo mtu hafanyi kazi kabisa au anafanya kwa kiwango kidogo lakini anazalisha kingi. Kama bado tuna pumzi inabidi kujiuliza...kwanini wawekezaji ni wachache angali ni sehemu ambayo mtu hafanyi kazi kubwa lakini kinachozalishwa ni kingi? Tutaongea na kujitetea mengi ila sababu kubwa ni ileile sababu ambayo watu wengi hawawezi kuanzisha biashara zao binafsi. Kwa ujumla tunaweza sema HOFU YA KUPOTEZA PESA(RISK)
Wengi hawataki kuona wala kusikia kuwa pesa yao waliyoitolea jasho haijaleta matunda waliyoyategemea wanachotaka kusikia ni “ ile laki moja imezaa laki tano mkuu” baaasi na sio “zile trei 80 za mayai ulizoziagiza kutoka Iringa nasikitika kukuambia kuwa nusu yamepasuka katika harakati za usafirishaji”. Wengi tunaogopa kupata hasara au kupoteza fedha zetu kiasi kwamba tunaamua tusiwekeze kabisa huku tukijisahaulisha kiasi gani cha pesa tungeweza kukizalisha kama mambo yangeenda vizuri.
Hofu ya kupoteza pesa inawagawanya wawekezaji katika nyanja nne:
(1) Wale ambao kwao hasara hawataki kuisikia na kuamua kutofanya chochote zaidi ya kuweka pesa benki au vibubu (aina yoyote ile ya kibubu) mpaka pale zitakapofika alizozitarajia.
(2) Wale ambao kazi ya kuwekeza wamewaachia watu wengine kama washauri wa mambo ya pesa waliosomea n.k
(3) Mbahatishaji/mcheza Kamari
(4 Mwekezaji
Tofauti ya mbahatishaji na mwekezaji ni rahisi tu, Mbahatishaji kwake kuwekeza ni mchezo wa bahati nasibu na MWEKEZAJI kwake kuwekeza ni mchezo wa kutumia akili/ujuzi. Na kwa wale ambao wamewakabidhi kazi ya kuwekeza watu wengine, kwao kuwekeza ni mchezo ambao hawataki kuujua kwahiyo wanapaswa kuchagua au kupata washauri wazuri. (Cha kufahamu hapa ni kwamba wengi waliosomea katika kushauri wengine masuala ya fedha kama kuwekeza, wao wenyewe hawaingizi pesa kupitia uwekezaji bali kupitia pesa utakayomlipa, wengi wameshindwa kufanya wanachowahubiria wengine)
Habari nzuri ambayo nataka nikufahamishe ni kwamba hii HOFU YA KUPOTEZA PESA unaweza kuipunguza kama sio kuiondoa kabisa na kuzalisha pesa nyingi kama tu utauelewa MCHEZO WA KUWEKEZA. Ujuzi unaotakiwa kuufahamu ili ufanikiwe katika uwekezaji unawezekana kujifunza kama tu utaamua na kujipa muda.
#TutawafikishiaHapa

No comments:
Post a Comment