elimuyautajiiri.blogspot.com

Sunday, March 31, 2019

SOMO LA ISHIRINI NA NANE @elimuyautajiri

Hawa ni wawekezaji pia ila ni wale ambao wako bize sana kiasi cha kuona kuwa hawana muda wa kujifunza UWEKEZAJI. Wengi ambao wako katika hili daraja ni wale waliosoma sana yaani wako bize na kazi zao (taaluma walizomea), familia au vitu vingine wanavyovipendelea hali kadhalika likizo wanazokuwa nazo kila baada ya muda fulani. Kwa hiyo kutokana ubize wao wanaona haina haja ya kujifunza uwekezaji na kuamua kuwakabidhi wengine wawafanyie huo uwekezaji. Mara nyingi wanawapa watu waliobobea katika eneo fulani wawawekezee huku wakibaki  kusali na kuomba usiku na mchana kuwa yule waliyemkabidhi aendeshe mambo vizuri.
Tatizo kubwa linaloambatana na hili daraja ni kwamba pale mtu atakapopoteza pesa au kupata hasara ya kiwango fulani hana anachojifunza. Hawapati somo lolote zaidi tu ya kupata somo baya kwamba usiwekeze kwenye jambo fulani utapoteza pesa zako bure. Ambacho watafanya zaidi ni kumlaumu yule jamaa waliyemkabidhi pesa, kulaumu soko au serikali (kwa jinsi inavyobadilisha kiwango cha kuwapa viinua mgongo vyao kwa wale walioajiriwa---hawa wamewapa serikali wawatunzie pesa). Fahamu kwamba ni ngumu kujifunza umekosea wapi kama hujui kosa gani limefanyika. 
#YouTubeSoon

Tembelea BLOG yetu kutuunga mkono... elimuyautajiri.blogspot.com

SOMO LA ISHIRINI NA SABA @elimuyautajiri


Hawa ni wale ambao kwao ili kuwa na pesa ya pamoja njia nzuri wameona ni kudunduliza/kusevu kidogo kidogo mpaka pale zitakapofikia kiwango walichokipanga. Udundulizaji wa pesa upo wa aina nyingi kuna wale ambao tutaamua kuweka pesa kwenye vibubu vya kawaida au siku hizi vibubu vya kwenye simu, kuweka benki au wengine kwa njia ya VIKOBA. Ubaya wa wengi kama sio wachache lengo la kudunduliza hivi ni kutaka kununua vitu tu vya kawaida vya nyumbani au urembo (kwa wanawake) mfano kununua dera jipya, simu nzuri zaidi n.k. Tunachotakiwa kufahamu ni kwamba si dhambi kudunduliza kama una malengo ya kuwa TAJIRI siku moja, bali ni dhambi kubwa kwa kudunduliza miaka nenda rudi kwa lengo la kununua vitu ambavyo havitakuingizia pesa. Tunachotakiwa ni kudunduliza na kutumia tutakachokipata kwa kununua vitu ambavyo vitatuingizia pesa au kufanya biashara. 
Kama na wewe unatunza pesa miaka nenda rudi kwa lengo la kununua kitu fulani ambacho hakitakuingizia pesa...basi nikuamshe tu.....UNAPOTEA. Ila kwa wewe ambae unadunduliza kwa lengo la kufanya biashara au kuna kitu unahisi ukikinunua kitakuingizia pesa basi HONGERA nyingi sana zikufikie popote ulipo ..nikwambie tu kuwa una mawazo ya KITAJIRI. 
Watunzaji wa kweli wa pesa wanatunza kwa ajili ya biashara au kwa ajili ya kununua vitu ambavyo vitawaingizia pesa. Ukinunua vitu vya kukuingizia pesa unaweza jikuta umerudisha pesa yako na kitu ulichokinunua bado kipo.
#YouTubeSoon

Tembelea BLOG yetu kutuunga mkono... elimuyautajiri@blogspot.com

Saturday, March 30, 2019

SOMO LA ISHIRINI NA SITA @elimuyautajiri





Asilimia nyingi tu ya wananchi wa Tanzania ni maskini wa kiwango cha kutokuwa na kiasi chochote kile cha kuwekeza. Wenyewe tunasema tupo katika kiwango cha kuishi kusogeza siku mbele tu.
Ila cha kushangaza ni kwamba kuna baadhi ya wale wanaotengeza pesa nyingi wanaingia katika daraja hili. Hawa wanazalisha kiasi kingi ila pia wanatumia zaidi ya wanavyozalisha. Kuna muda mtu anaweza kuonekana TAJIRI sana. Ana mke mzuri, watoto watatu na wote wakawa wanasoma shule za kulipia (private schools). Yeye na mkewe wakawa wanaendesha magari ya kifahari. Na huenda akawa anakaa na familia yake katika jumba zuri kabisa na watoto wakikua wanaendesha magari ya kifahari pia. Machoni mwa watu wengi mtu kama huyu anaonekana ni TAJIRI sana lakini kumbe kiuhalisia  huenda wakawa na madeni makubwa na ni maskini kuliko wale tunaowaona sisi ni maskini. Ukweli mchungu ni kwamba wengi wao kama sio wachache sio wawekezaji kwa maana hawana wanachokiwekeza.
(Naomba nisieleweke vibaya hapa---tukirejea maana ya WAWEKEZAJI ni wale wanaozalisha pesa zao kupitia vyanzo mbalimbali walivyowekeza bila ushiriki wao au ushiriki  wao mdogo na sio wale wanazalisha pesa nyingi kupitia mishahara n.k). Baadhi kati ya wengi  wanaomiliki magari...wananunua kupitia mishahara yao na si kutokana na UWEKEZAJI wao. Yaani siku mshahara ukikata tu tutaanza kutafutana. TUWEKEZE 
Pia tuchukulie mfano wa msanii wa muziki yeyote yule ambaye anafanya vizuri kwenye muziki...wengi kama sio wote huwa wanaendesha magari na kuishi katika majumba ya kifahari n.k....Umegundua huwa inakuaje pale ambapo jina lake linapotea kwa muda au linapopotea daima....wengi wao wanaangukia katika dimbwi la umaskini kwa kuwa hawana vyanzo ambavyo wamewekeza na ambavyo vitazalisha bila hata ya uwepo wao....wengi wanategemea SHOW nyingi ndio ziwazalishie pesa na kusahau kuwekeza wanapozipata pesa hizo. 
Tunachokipongeza kwa sasa wasanii wa kwetu hapa Tanzania wameamka.... @jumajux @mwanafa @vanessamdee @diamondplatnumz @officialalikiba wote hawa wamewekeza na tunazifahamu bidhaa zao....bila kuwasahau na wengine wengi ambao wamewekeza kwa ajili ya maisha ya baadae. HONGERA KWAO...Wakiendelea kuwekeza wataishi maisha ya kifahari milele.

SOMO LA ISHIRINI NA TANO @elimuyautajiri



Bwana Robert Kiyosaki amegawanya wawekezaji katika madaraja/aina tano: (1) Ambao HAWANA KABISA CHA KUWEKEZA
Pia daraja hili linahusisha baadhi ya wanaotengeneza pesa nyingi. (2) WATUNZAJI WA PESA (wale wa kusevu—savers)
Wale wa kuweka pesa benki, kwenye vibubu, wanaosubiria kupata viinua mgongo wakistaafu n.k (3) Ambao WAKO BIZE SANA. 
Hawa ni wale ambao kazi ya kuwekeza wamewaachia wengine kwa kuwa wako bize sana kiasi cha kushindwa kujifunza uwekezaji. (4) Ambao WANAONA WANAWEZA  KUFANYA KILA KITU WENYEWE.
Wengi ya waliostaafu wanaingia katika aina hii ya wawekezaji (5) WAMILIKI WA BIASHARA WALIOAMUA KUWEKEZA
Tukikumbushana kuwa hawa sio waliojiajiri katika biashara zao bali wanaomiliki biashara (B) wakaamua kuwekeza (I). Na hapa ndipo ambapo tunashauriwa kulenga kama tunawaza kuwa WAWEKEZAJI siku moja.

Tuendelee kuwa pamoja tutakuchambulia kwa kirefu kila daraja la wawekezaji.
#MjulisheNaMwingineAfaidike

Attachments area

Sunday, March 24, 2019

TANGAZO TANGAZO TANGAZO (YOUTUBE CHANNEL NA APP YA ELIMU YA UTAJIRI)

MPENDWA MDAU WA BLOG YETU ASANTE KWA KUENDELEA KUTUFATILIA NA KUFATILIA MASOMO YETU.
TUNAFURAHA KUKUTAHARIFU KUWA KWASASA TUNA PATIKANA YOU TUBE NA PIA TUNA APP YETU AMBAPO KWANJIA HIZI ZOTE UTAWEZA KUENDELEA KUFATILIA MASOMO YETU KWA KUSOMA LAKINI PIA KWA KUSIKILIZA NA KUTAZAMA VIDEO.

UNACHOTAKIWA KUFANYA NI KUSUBSCRIBE CHANELL YETU YA YOUTUBE INAYOITWA ELIMU YA UTAJIRI LAKINI PIA KUINSTALL APP YETU YENYE MASOMO YOTE, LINK ZOTE TUMEKUWEKEA HAPO CHINI.

GUSA HAPO CHINI KWENDA MOJA KWA MOJA YOUTUBE KUSUBSCRIBE CHANELL YA ELIMU YA UTAJIRI NA KUONA VIDEO ZETU.

👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇


GUSA HAPO CHINI KUDOWNLOAD NA KUINSTALL MOJA KWA MOJA APP YETU YA ELIMU YA UTAIJIRI KWENYE SIMU YAKO.

👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇

SOMO LA ISHIRINI NA NNE @elimuyautajiri



UWEKEZAJI ni jambo muhimu sana ili kuwa na UTAJIRI wa kweli. 
Vitu vitano huwatokea ambao hawawekezi au ambao huwekeza bila maarifa ya kutosha:
(i) Hulazimika kufanya kazi maisha yao yote (ii) Wanakuwa na hofu ya pesa maisha yao yote.
(iii) Wanawategemea wengine kama familia, kampuni au serikali katika maisha yao yote.
(iv) Pesa huweka mipaka ya maisha yao ( mf. Siwezi mpeleka mwanangu shule binafsi kwa kuwa sina pesa)
(v) Hawataelewa kamwe nini maana ya uhuru wa kweli (uhuru wa kipesa--utajiri wa kweli)

UNAJIULIZA UWEKEZE KWENYE NINI UFANIKIWE?
Basi unachotakiwa kukifahamu ni kwamba kujiuliza kila siku uwekeze kwenye nini ili ufanikiwe halitakiwi kuwa swali lako tena kuanzia leo. Unachotakiwa kujiuliza ni je, wewe ni mwekezaji mzuri?. Mwekezaji mzuri ni yule ambae ana maarifa ya kutosha juu ya kitu anachokifikiria kuwekeza ikimaanisha kuwa  ana ufahamu juu ya mtaji unaohitajika, changamoto zinazoambatana, jinsi ya kuzikabili na mengine mengi.

Hakuna uwekezaji fulani ambao kila atakayeamua kuwekeza eneo hilo atafanikiwa ..hatuoni leo watu fulani wamewekeza katika afya, kilimo, maduka, mitandao ya simu n.k wakafanikiwa sana... lakini kuna wengine tunajaribu humo humo leo kesho lakini hatufanikiwi? Basi jua unachotakiwa ni kutafuta maarifa ya kutosha juu ya kile unachofikiria kukiwekeza. Sidhani kama kuna mtu yeyote hana walau kitu kimoja kichwani kwake anachokifikiria kuwekeza. 
Hivi hatujawahi kusikia kuna watu wamejiapiza kabisa kuwa hawatawekeza kamwe kwenye biashara ya nyanya kwa kuwa nyanya huchukua muda mchache sana kuharibika? Na je hatujawaona watu wengine wakiendesha maisha ya familia zao na kuishi vizuri kwa sababu ya biashara hiyo hiyo ya nyanya ambayo yule mwingine ameapa kutoifanya maishani? Hapo ndipo utakapoiona nguvu ya maarifa katika uwezekezaji. 
Maarifa juu ya kile unachotaka kukifanya unaweza kuyapata kupitia:
--Kukutana na waliotangulia kufanya kitu hicho
--Kusoma vitabu na majarida mbalimbali
--Kusoma mtandaoni juu ya hiko kitu n.k
#KilaLaKheriTaifaStars
#YouTubeSoon

Tuunge mkono kwa kutembelea 

SOMO LA ISHIRINI NA TATU @elimuyautajiri



Kama kweli unataka kufanikiwa basi unatakiwa kuondoa HOFU YA KUKATALIWA na pia USIJALI MANENO YA WATU JUU YAKO. Hofu ya kukataliwa inaeleweka sana na wengi kwenye suala la mapenzi ambapo mtu anapohitaji kuwa na mtu fulani kimapenzi anakuwa na hofu kubwa kuwa huenda akakataliwa na mwisho wa siku anaamua aache kueleza ukweli wa moyo wake. Hofu ya kukataliwa inaonekana sehemu nyingi sana na imekuwa ikiwafelisha wengi kufikia ndoto zao...mfano, wengi tunashindwa katika mahojiano (interview) mengi kutokana na kuwa na hofu hii yaani mtu anaanza kutoka jasho kabla hata hajaingia kwenye chumba chenyewe au hata akiingia atakachokiongea hata mwenyewe akitoka nje atashangaa kwa nini imekuwa vile. 
Hofu hii hupelekea mambo mengi kama hofu ya kukutana na watu wapya yaani mtu anaona ni kitu kigumu sana kuzungumza na mtu mpya au rafiki wa marafiki zake, na kwa vijana wengi walio vyuoni au maeneo mbalimbali ya elimu huwa na makundi yao  yaani marafiki wa aina fulani na inabidi wafanye kama wenzao wanavyofanya hata kama vitu hivyo ni vibaya kwa kuwa wanaogopa huenda wenzao wakawakataa (wanasemaga hauna swaga kama zetu) n.k .

Pia usisahau mambo kama kutaka kuonekana na tabia fulani katika jamii wakati sio ukweli wa tabia yako, kutaka kumridhisha kila mtu, kushindwa kusema unachokihitaji ingawa unakihitaji sana n.k ni baadhi ya tabia zinazoletwa na HOFU YA KUKATALIWA.
USIJALI MTAZAMO/ MANENO YA WATU juu yako yakakusahaulisha ndoto zako. Wengi tunashindwa kufanya vitu tukihofia marafiki watasema nini endapo tutaamua kufanya vitu tofauti. Naomba nitolee mfano wa wanachuo, mwanachuo akipata somo la uwekezaji leo hii na akaamua kubadilika wengi watashindwa kufanikisha suala la uwekezaji na kikubwa zaidi ni maneno ya wenzake kama "huyu jamaa sio mjanja kabisa yaani mavazi yake sio ya kichuo chuo" wakimaanisha kwamba mwanachuo lazima uwe na kiatu kizurii na modo nzuri iliyoshika mwili vilivyo, uwe na unyoaji ambao labda wasanii pekee ndio wananyoa au uwe na suruali inaonyesha mwili ipasavyo au mshono wa kitenge wa kipekee au bei kubwa ambayo huenda hukuwahi kuuwazia kabla hujafika chuo (kwa wanawake) n.k. Basi mambo kama hayo huwafelisha wanachuo na wengine wengi mtaani.
#YoutubeSoon

Friday, March 22, 2019

SOMO LA ISHIRINI NA MBILI @elimuyautajiri


Leo nimekumbuka ile stori ambayo baba alinisimulia kuwa dada yangu na wanafunzi wenzake walifeli somo la hisabati ingawa walikuwa na mwalimu mzuri (kwao walimuona MBAYA). Baba alidai kuwa dada na wenzake walipeleka ombi kwa mkuu wa shule kuwa hawamtaki mwalimu wao mpya wa Hisabati (Mathematics) kwa kuwa alikuwa akiwachapa sana waliopata maksi chache na alikuwa anapenda kuingia darasani hata kama kipindi sio chake. Mwisho wa stori sikumbuki ilikuwaje kama mwalimu alihama shule au alibadilishiwa kidato ila ninachokumbuka kuwa mwaka aliomaliza dada yangu walifeli sana somo hilo.
Turudi katika mada yetu….MAFANIKIO tunaweza kuyafananisha na huyo mwalimu hapo juu, MAFANIKIO huchapa bakora sana kuliko hata mwalimu aliekua anatuchapa sana bakora tulivyokuwa shuleni. Adhabu ambazo mafanikio yatakutaka uzipitie ni chaguo lako kuzikubali na kuzikabili au kuachana nazo kama ambavyo dada yangu na wanafunzi wenzake walivyofanya.
Ninachokimaanisha hapa ni kwamba tunatakiwa kukubaliana hali kadhalika kukabiliana na  changamoto mbalimbali ambazo zitatutokea katika harakati za kutaka kufanikiwa.
Unaweza ukapoteza biashara mbili au tatu kabla ya kupata moja ambayo ikakupa mafanikio na kukusahaulisha shida zako milele. USIKATE TAMAA kama limekutokea hili au kama litakutokea hili katika kupambana kwako. Tunajifunza mengi sana pale tunapofeli kuliko tunapofaulu, kwa hiyo usiogope kufeli.Kufeli ni hatua mojawapo ya  mafanikio. Huwezi pata mafanikio bila kufeli. 
Tuunge mkono kwa kutembelea... elimuyautajiri.blogspot.com


Tuesday, March 19, 2019

SOMO LA ISHIRINI NA MOJA @elimu_ya_utajiri



Tuanze kwa kuangalia mfano hai ambao unaweza tokea au hutokea katika maisha yetu ya kawaida. Tuseme leo kampuni unayoifanyia kazi inauzwa na boss anaekuja ni mpya. Kiuhalisia sio kwamba wote mliokuwa mnafanya kazi chini ya boss wa mwanzoni mtaendelea kuwa na kazi baada ya kuingia bosi mwingine.Wengi tutaishia kulia machozi ya damu kwa kuwa kukosa kazi kwa wengi wetu kunamaanisha maisha yatakuwa magumu. Unajua kwa nini wengi tutalia? Hii ni kwa sababu wengi tuliwaza kufanikiwa kutokana na mshahara au tunaweza sema tulikuwa tunategemea mshahara utufanye kuwa MATAJIRI siku moja…hii ina maanisha kwamba ulikuwa unamtegemea boss wako akufanye uwe TAJIRI..wengi tunasahau kuwa jukumu la boss ni kutupa MSHAHARA tu …ila kama unataka kuwa TAJIRI ni jukumu lako wewe mwenyewe na hili huanza pale tu unapoanza kupokea MSHAHARA.
Kama hauna maarifa  ya kutosha katika kuzitawala pesa zako, pesa za kiwango chochote hazitakunusuru na janga la umaskini. Kama utabajeti pesa yako vizuri na kupata maarifa ya kumiliki biashara kubwa kubwa au uwekezaji basi utakuwa upo katika njia ya kuwa TAJIRI.Tunatakiwa kufahamu  tofauti kubwa iliyokuwepo kati ya TAJIRI na maskini  ni jinsi wanavyotumia muda wao  ambao wanakuwa huru (FREE). Wengi tuko bize tukihangaika na mshahara tukasahau kujenga kesho yetu, kama utakuwa bize na mshahara basi utakuwa bize maishani. Ila kama unataka kuwa bize basi ni bora ukawa bize kwa yote mawili yaani mshahara au kujiajiri na kuhangaika kuwa na biashara kubwa au kuwekeza. 

Ila tunashauriwa kabla hatujawa wawekezaji inabidi tuanze kuhangaika kumiliki biashara kubwa kubwa/ kupanua biashara. Kwa nini? Hii ni kwa sababu ya kujipa muda wa kutosha kupata UZOEFU NA ELIMU hali kadhalika KUHAKIKISHA TUNAKUA NA MZUNGUKO MZURI WA PESA kwa maana uwekezaji una kupata au kukosa kwa hiyo kama ukiwa na mzunguko mzuri wa pesa hata kama utakosa mara moja mara mbili utaweza kujipanga tena kwa mara ya tatu na ya nne. Wengi ya tulioajiriwa au kujiajiri tuko katika hali mbaya kiasi kwamba hatutaki kukosa walau mara moja katika uwekezaji wetu na ndio maana tunashauriwa kutengeneza mzunguko mzuri wa pesa kwanza.

                      DOWNLOAD APP YETU HAPA

SOMO LA ISHIRINI @elimu_ya_utajiri



Wengi ambao tunaamua kujiajiri mara nyingi hupenda kama sio kulazimika kwa kuanza na biashara ndogo ndogo. Katika biashara hizo huwa tunajitahidi kuwa kila kitu ili biashara isonge mbele kama vile kujibu simu zinazopigwa na wateja, kulipia bili mbalimbali, kupiga simu, kujaribu kutangaza biashara kwa bajeti ndogo, kuwahudumia wateja, kufukuza kazi wasaidizi wetu tunaoona wanafanya ovyo, kuwaajiri wasaidizi wengine, kuchukua nafasi ya wasaidizi wetu kama hawajatokea siku fulani ya kazi n.k...mfano mzuri unaweza kuwa mama ntilie, waliojiajiri kwa kufungua duka na wengine wengi.
Hivi ujawahi kusikia kijana fulani aliwekeza wekeza na kuazima kwa ndugu zake kiasi fulani cha pesa ili kimsapoti katika kuanzisha biashara yake mwenyewe halafu baada ya miaka mitatu au zaidi biashara ikaanza kwenda ovyo na badala ya kufanikiwa (kutoboa)  kama alivyowambia wenzake...... anabaki na deni? 
Unaambiwa biashara 9 kati ya 10 za namna hii hufeli baada ya miaka mitano. Na zile zilizofanikiwa kubaki 9 katika ya 10 hufeli baada ya miaka mitano mingine. Kifupi biashara 99 kati ya biashara ndogo ndogo 100 hufeli baada ya miaka 10.

Wengi hufeli ndani ya miaka mitano ya kwanza kutokana na kukosa uzoefu (experience) na mtaji. Na sababu ya kufeli kwa yule aliyefaulu miaka mitano ya kwanza sio kutokana na mtaji bali ni kutokana na  kuishiwa nguvu. Masaa mengi na juhudi kubwa wanazotumia katika majukumu yao kila siku ndani ya muda mrefu huwachosha na kufikia hatua mwili kuhitaji kupumzika....na hapo ndipo utakapokuta mtu anakosa juhudi kama zile alizokuwa nazo miaka iliyopita. Mfano kwa muuza duka, huchoka tena kuamka saa 12 kufungua duka kila siku na kwenda kulala saa 4 usiku au zaidi kama alivyokuwa anafanyaga zamani.... Na wanaofanikiwa kubaki hata ndani ya hiyo miaka kumi basi ni wale ambao wameendana na ile adha ya kuamka kila siku asubuhi, kwenda kazini na kufanya kazi kwa bidii maisha yao yote. Na mara nyingi  inaonekana hiko ndicho pekee wanachokifahamu maishani na ambacho wameamua kukifanya. TUANZISHE BIASHARA ILA SIO ZA MTINDO HUU....TUTAFELI....YATUPASA TUANGALIE MBALI ZAIDI
Attachments area

SOMO LA KUMI NA TISA @elimu_ya_utajiri




Baada ya kuona hali za wastaafu wengi wa serikalini na wengine baada ya kuwaona watu wengi waliojiajiri wakipata tabu sana pale wanapopata ugonjwa au wanavyoendesha maisha yao ya kila siku bila hata kupumzika, sasa tunajikuta tunalazimika kuwekeza bila ya kuwa na ELIMU YA UWEKEZAJI. 
Na wengi waliokuwa wanaogopa kupoteza pesa zao (RISK) kipindi wanafanya kazi wanalazimika kufanya kile kile walichokiogopa wakistaafu....Hivi hatuwashuhudii wafanyakazi wengi wakihangaika kutafuta miradi ya kuwekeza wakishastaafu? Kama kweli tunaogopa kupoteza pesa kwa nini sasa tuko tayari kuwekeza ukifikia muda wa kustaafu? Naweza sema...Mshahara wa kila mwezi kwa upande wa wafanyakazi na afya njema na umri kwa upande wa watu waliojiajiri vinatudanganya.... TUAMKE. 
Na kama hautafahamu leo haya ninayokwambia basi subiri mpaka pale utakapostaafu au umri utakapoenda uje uieleze ukweli dunia wewe mwenyewe. 
Ili uwe mwekezaji lazima uwe mwekezaji......hii inamaanisha lazima uwe na elimu ya uwekezaji ili uweze kujiita wewe ni MWEKEZAJI. Tatizo wengi ya waajiriwa na waliojiajiri asili yetu ni kutaka uhakika wa maisha (mshahara) na  ndio maana tunatafuta kazi au kuanzisha biashara  ndogondogo tunazoweza kuzimudu (waliojiajiri). Kwa kuwa wengi tumeshazoea uhakika wa maisha.....basi hata tunapotaka kuwekeza tunakuja kwa lengo la kutafuta uhakika huo huo, kumbe sio kweli kuwekeza ni sehemu ambayo inahusisha sana HOFU YA KUPOTEZA PESA(RISK) kuliko ule uhakika ambao wengi wetu tunaufuata. Kwa kufuata huu uhakika basi hili ni moja ya jambo ambalo wengi tunalifanya huku hatujui kama tunakosea:

KUWEKEZA KATIKA MAENEO MENGI
Wengi tunaamua kuwekeza maeneo mengi ili kuhakikisha kwamba hatupotezi pesa zetu.....yaani mtu atafungua duka la bidhaa ya chakula, atanunua boda boda,atauza nguo n.k.... yaani ili mradi tu ahakikishe huku kukienda vibaya basi huku kunaenda vizuri. Uwekezaji haushauri hivyo bali unashauri tafuta sehemu chache za kuwekeza halafu elekeza nguvu zako na akili zako huko na ukabiliane na kila hali. Wawekezaji waliofanikiwa au MATAJIRI hawafanyi hivyo bali wanaweka nguvu sehemu chache. 
KIKUBWA KATIKA KUWEKEZA INABIDI TUSIENDE NA MAWAZO YA KUOGOPA KUPOTEZA PESA.
#WhatsappNoSoon

SOMO LA KUMI NANE @elimu_ya_utajiri



Kuwekeza ni sehemu ambayo mtu hafanyi kazi kabisa au anafanya kwa kiwango kidogo lakini anazalisha kingi. Kama bado tuna pumzi inabidi kujiuliza...kwanini wawekezaji ni wachache angali ni sehemu ambayo mtu hafanyi kazi kubwa lakini kinachozalishwa ni kingi? Tutaongea na kujitetea mengi ila sababu kubwa ni ileile sababu ambayo watu wengi hawawezi kuanzisha biashara zao binafsi. Kwa ujumla tunaweza sema HOFU YA KUPOTEZA PESA(RISK)
Wengi hawataki kuona wala kusikia kuwa pesa yao waliyoitolea jasho haijaleta matunda waliyoyategemea wanachotaka kusikia ni “ ile laki moja imezaa laki tano mkuu” baaasi na sio “zile trei 80 za mayai ulizoziagiza kutoka Iringa nasikitika kukuambia kuwa  nusu yamepasuka katika harakati za usafirishaji”. Wengi tunaogopa kupata hasara au kupoteza fedha zetu kiasi kwamba tunaamua tusiwekeze kabisa huku tukijisahaulisha kiasi gani cha pesa tungeweza kukizalisha kama mambo yangeenda vizuri.
Hofu ya kupoteza pesa inawagawanya wawekezaji katika nyanja nne:
(1) Wale ambao kwao hasara hawataki kuisikia na kuamua kutofanya chochote zaidi ya kuweka pesa benki au vibubu (aina yoyote ile ya kibubu) mpaka pale zitakapofika alizozitarajia.
(2) Wale ambao kazi ya kuwekeza wamewaachia watu wengine kama washauri wa mambo ya pesa waliosomea n.k
(3) Mbahatishaji/mcheza Kamari
(4 Mwekezaji

Tofauti ya mbahatishaji na mwekezaji ni rahisi tu, Mbahatishaji kwake kuwekeza ni mchezo wa bahati nasibu na MWEKEZAJI kwake kuwekeza ni mchezo wa kutumia akili/ujuzi.  Na kwa wale ambao wamewakabidhi kazi ya kuwekeza watu wengine, kwao kuwekeza ni mchezo ambao hawataki kuujua kwahiyo wanapaswa kuchagua au kupata washauri wazuri. (Cha kufahamu hapa ni kwamba wengi waliosomea katika kushauri wengine masuala ya fedha kama kuwekeza, wao wenyewe hawaingizi pesa kupitia uwekezaji bali kupitia pesa utakayomlipa, wengi wameshindwa kufanya wanachowahubiria wengine)
Habari nzuri ambayo nataka nikufahamishe ni kwamba hii HOFU YA KUPOTEZA PESA unaweza kuipunguza kama sio kuiondoa kabisa na kuzalisha pesa nyingi kama tu utauelewa MCHEZO WA KUWEKEZA. Ujuzi unaotakiwa kuufahamu ili ufanikiwe  katika uwekezaji  unawezekana kujifunza kama tu utaamua na kujipa muda.
#TutawafikishiaHapa

SOMO LA KUMI NA SABA @elimu_ya_utajiri





Ukiachana na umuhimu wa elimu (SHULE) katika maisha ya binadamu,  watu wengi tumeamua kuwekeza katika elimu kuliko sehemu nyingine yoyote. Uwekezaji katika elimu unahusisha miaka yote mtu anayoitumia kutoka shule ya msingi, sekondari, elimu ya juu mpaka muda ambapo mtu atakuwa anafanya kazi. Wawekezaji wengi wa elimu wanategemea kuzalisha  pesa nyingi pale watakapoongeza elimu zaidi, mfano mwalimu wa ngazi ya  Stashahada (diploma) anapoenda kusoma zaidi ili apate Shahada (Degree) n.k
Kufanya kazi kwa bidii na uaminifu kwa mwajiri wako ni aina nyingine za  uwekezaji ambayo pia wengi tumeichagua.Na kupitia hiyo kazi tunapata uhakika wa viinua mgongo hapo baadae na huduma zingine kupitia mikataba yetu na mabosi wetu
Uwekezaji mwingine ni ule wa kuwa na watoto wengi ili baadae wakuhudumie ukiwa mzee. Kwa bahati mbaya siku hizi maisha yamewaendea mrama watoto wengi kiasi kwamba wameshindwa kuzimudu gharama za maisha na afya za wazazi wao.
Ingawa hiyo iliyotangulia juu ni mifumo mbalimbali ya uwekezaji…uwekezaji mzuri na wa kweli ni ule ambao unakuzalishia kipindi ambacho unaendelea kufanya kazi na sio ule wa kupata pesa zako ukishastaafu. Unataka kuwa mwekezaji wa namna hii..basi jiulize..Je, unaingiza pesa kupitia uwekezaji? Au kwa maneno mengine unaweza kujiuliza..Je, pesa yako inakutumikia na kukuzalishia kipato chako cha sasa hivi?
Tuangalie mfano wa mtu aliyeamua kuwekeza kwa kununua nyumba na kuamua kuipangisha. Kama kodi anayoipokea inazidi gharama za uendeshaji wa ile nyumba basi mtu huyo anaingiza pesa kupitia uwekezaji (eneo I). Au yule ambaye aliamua kununua BODA BODA akampa mtu aendeshe halafu ikawa inazalisha pesa zaidi ya gharama za uendeshaji wake…basi mtu huyo anazalisha pesa kama mwekezaji (TUTASOMA AINA TOFAUTI ZA WAWEKEZAJI). Kwa hiyo ili ujiite MWEKEZAJI (I) ni lazima kuangalia kiasi gani cha pesa unachozalisha eneo lolote (E, S au B) bila ya kufanya kazi katika eneo hilo.

SOMO LA KUMI NA SITA @elimu_ya_utajiri



Katika makala ambayo aliisoma bwana Robert Kiyosaki anatuambia kuwa ilikuwa inaonesha kwamba asilimia 70 ya kipato cha matajiri kinatokana na vyanzo mbalimbali walivyowekeza na asilimia chini ya 30 ndio inayotoka kwenye mshahara, na kama waliajiriwa basi ni wafanyakazi katika kampuni zao. 
Kwa watu wengine, maskini na watu wa daraja la kati... karibia asilimia 80 ya kipato chao kinatokana na mshahara (kuajiriwa au kujiajiri) na chini ya asilimia 20 kutoka kwenye vyanzo walivyowekeza. (HAPA NI CHANGAMOTO KWETU KAMA TUNATAKA KUWA MATAJIRI SIKU MOJA…INATUPASA TUPAMBANE TUFIKIE  WALAU ASILIMIA 70 KUTOKA KWENYE UWEKEZAJI WETU)-------MUNGU ATUJALIE

NINI MAANA YA UTAJIRI?
Wengi wetu tunafahamu kuwa TAJIRI ni mtu mwenye pesa nyingi au mtu anayetengeneza pesa nyingi kwa mwezi. Ila UTAJIRI hautazamwi kwa kuangalia kiasi cha pesa unachozalisha kwa mwezi au kiwango cha pesa ulicho nacho….UTAJIRI unaangaliwa kwa idadi ya siku ambazo utaweza kuishi bila ya wewe au mtu yeyote katika familia yako kufanya kazi. Kwa mfano, matumizi yako au ya  familia yako ni laki 2 (200,000/=) kwa mwezi na wewe katika akiba yako una sh. Milioni moja (1,000,000/=) manake UTAJIRI wako ni wa miezi mitano (5) au siku 150 tu.

Kinachotakiwa ni kuhakikisha kuwa tunawekeza mpaka kufikia mahali ambapo vipato vyetu kwa mwezi vinazidi matumizi yetu. Kwenye suala la  UTAJIRI shida sio kiasi gani cha pesa unachokizalisha kwa mwezi.....bali ni kiasi gani ambacho utaendelea kuwa nacho na kwa muda gani pesa hiyo itaendelea kukutumikia.
Watu wengi leo inawezekana wanatengeneza pesa nyingi lakini yote inaishia kwenye matumizi na kila muda wanapozalisha zaidi wanazidisha tena matumizi.
Kumbuka....Moja ya matatizo makubwa yanayotukumba watu wengi siku hizi ni mawazo (STRESS)  yanayotokana na kufanya kazi kwa bidi lakini bado vipato havikidhi mahitaji (MATUMIZI)
#MjulisheMwingineKuhusuPageHii
#MatajiriWaKesho

SOMO LA KUMI NA TANO @elimu_ya_utajiri



Leo tutamalizia watu wa mwisho katika jedwali la mzunguko wa pesa wanaojulikana kama wawekezaji (Investors-I). Hawa ni watu wanaotengeneza pesa kupitia pesa, hawana haja ya kufanya kazi tena mana pesa inawafanyia kazi. Eneo I ni eneo ambalo MATAJIRI wa ukweli wanapatikana, hata kama unatengeneza pesa eneo lingine lolote (E, S, au B), kama kweli unautaka utajiri fanya hima ufike eneo I ambapo pesa itakuzalishia pesa zaidi. Fanya kazi zako za kila siku ukilenga siku moja kufika hapa. Hili ni eneo ambalo pesa inabadilika na kuwa UTAJIRI.
JEDWALI LA MZUNGUKO WA PESA
Hili limetutofautishia maeneo mbalimbali tunayozalisha pesa zetu, kwa kifupi tu:
(1) E wanapata vipato vyao kupitia ajira
(2) S wanamiliki kazi/ajira (wamejiajiri)
(3) B wanamiliki MFUMO WA BIASHARA na wana watu wanawafanyia kazi
(4) I pesa inawafanyia kazi/ wanaitumikisha pesa
Siri kubwa ya kupata utajiri ni KUTUMIA MUDA NA PESA ZA WATU WENGINE na hili linawezekana tu endapo utakuwa katika eneo B na I. Kwa kiwango kikubwa watu ambao wapo E na S ndio wale watu wengine ambao PESA NA MUDA WAO unatumika.
KWA NINI TUTOKE E  na S?
Moja ya ubaya wa kufanikiwa katika kazi uliyojiajiri (S) ni kwamba mafanikio yako yanamaanisha kufanya kazi kwa bidii zaidi na kwa muda mrefu zaidi. Tuangalie mfano wa yule daktari bingwa wa meno…kufanikiwa kwake au kuingiza kwake pesa nyingi zaidi manake awe na wateja karibu muda wote ndani ya masaa 24…yani kama ingewezekana ili ajihakikishie pesa nyingi zaidi kwa siku ahudumie hata masaa 24 YOTE Je, haya ni mafanikio ya kweli?….Na vipi kuhusu kinyozi? Mafanikio yake yakoje? Na Machinga je? Sio kwamba kila Machinga anatamani siku nzima iwe mchana? ili atengeneze pesa zaidi.....?? Ila ukiwa B mafanikio zaidi yanamaanisha nini? BIASHARA zako zimepanuka zaidi na umeajiri watu wengi zaidi wa kukufanyia kazi. Kwa maneno mengine tunasema unafanya kazi kidogo, unazalisha kingi zaidi na unapata muda mwingi zaidi wa kuwa HURU (FREE TIME)
JAMANI TUPAMBANE TUTOKE (E na S) SIKU MOJA

SOMO LA KUMI NA NNE @elimu_ya_utajiri



Wale ambao wanamiliki biashara wanaweza kwenda mbali na biashara zao kwa muda hata wa mwaka mmoja au zaidi na watakaporudi wakakuta biashara zao zimeingiza faida zaidi na zinaenda vizuri kuliko walivyoziacha. Ila kwa mtu aliyejiajiri katika biashara yake akitoka ndani ya mwaka au zaidi, kuna asilimia kubwa kuwa hakutakuwa na biashara tena.
UTOFAUTI UKO WAPI?
Kwa kifupi tu tunaweza sema kuwa huyu aliyejiajiri anamiliki KAZI na huyu anayemiliki biashara tunasema anamiliki MFUMO WA BIASHARA na kuajiri waliobobea katika maeneo tofauti kuendesha biashara zake. Au kwa maneno mengine tunaweza sema mara nyingi huyu aliyejiajiri yeye ndio mfumo wenyewe yaani yeye ndio kila kitu na ndio maana hawezi KUONDOKA.
Tuchukue mfano mzuri wa daktari bingwa wa meno, tuseme kasoma miaka mingi tu mpaka kupata taaluma hiyo halafu akaamua kujiajiri kwa kuwa na sehemu yake ya kutoa huduma. Wewe kama mteja ukaenda kwa tatizo lako akakuhudumia vizuri sana, lazima utawatangazia marafiki na watu wengine wakikuuliza kuhusu tatizo la meno. Mara nyingi madaktari bingwa wa meno wanaweza kufanya kazi yote kuhusiana na meno wao wenyewe kwa msaada wa manesi wachache labda. Tatizo linakuja pale ambapo daktari huyo atakapoamua kwenda likizo, akienda likizo basi na kipato chake kitaenda likizo kwa maana hataingiza tena pesa mpaka pale atakaporudi.
Wamiliki wa biashara (B) wanaweza kwenda likizo maisha yao yote kwa kuwa wanamiliki MFUMO WA BIASHARA na sio KAZI. Hata B (Business owner-mmiliki wa biashara) akienda likizo pesa inaendelea kuingia. Ukitaka kufanikiwa ukiwa eneo B lazima: (1) umiliki mfumo wa biashara (2)Uwe na uwezo wa kuwaongoza wengine
Kwa wale tuliojiajiri katika biashara (S) ili kuwa wamiliki wa biashara (B) tunatakiwa tubadilike tusiwe kila kitu katika biashara zetu, kibaya zaidi wengi wetu TUNASHINDWA kufanya ivo.
#KamaUnatakaKuwaTajiriBadilishaMtazamo
#MabadilikoYanaanzaNaKujuaWapiUlipo
#MatajiriWaKesho
#MjulisheNaMwingine

SOMO LA KUMI NA TATU @elimu_ya_utajiri



Kundi hili linaweza kuwa kinyume kabisa na lile la S, watu ambao wamebobea katika kundi B wanapenda kujiweka karibu sana na watu walio vizuri katika maeneo tofauti ya E, S, B na I. Hawa sio kama wale wa S ambao hawapendi  kuwapa kazi  wengine wakiamini kwamba hakuna anaweza kufanya zaidi yao. B wanapenda kuwapa kazi wengine. Kauli mbiu ya watu hawa ni “KWANINI UFANYE MWENYEWE WAKATI UNAWEZA KUAJIRI WENGINE WAKAFANYA KWA AJIRI YAKO NA WAKAFANYA VIZURI?
UONGOZI MZURI NI SUALA MUHIMU KATIKA ENEO B
“UONGOZI ni ule uwezo wa kumshawishi mtu afanye kazi kwa ubora wake wote alionao”. Uongozi mzuri na maarifa ya biashara ni mambo muhimu sana katika eneo B. Inaonekana wengi wana kitu kimoja  kati ya hivyo viwili.. utakuta mtu ana maarifa mazuri tu ya biashara fulani lakini kwa upande wa kuwaongoza watu wake inakuwa tabu au mwingine anajua kuongoza watu vizuri tu lakini hana maarifa ya kutosha ya biashara husika. Ila tambua ili uweze kuwa na mafanikio makubwa katika eneo B lazima uwe na mambo yote mawili na cha kukutia moyo ni kwamba vyote viwili unaweza kujifunza na ukawa vizuri. Maarifa ya uongozi na biashara ni endelevu hayana mwisho kila siku yapasa uendelee kujifunza kutokana na kukutana na watu mbalimbali na pia mabadiliko ya kila siku yanayotokea katika dunia ya leo.

Maarifa kama kusoma taarifa ya biashara, kuangalia masoko ya biashara yako, jinsi ya kuweka makubaliano na wengine, jinsi ya kufanya matangazo ya biashara yako n.k ni mambo ambayo ni rahisi kujifunza. Kwa wengi shida inakuja kwenye suala la kufanya kazi na wengine halafu mambo yakaenda sawa (UONGOZI). UJASIRIAMALI
Wengi tunawasikia wakisema “nataka kuanzisha biashara yangu mwenyewe”. Wengi tunaamini kuwa ili tuwe na uhakika wa pesa na maisha yenye furaha basi inabidi kuanzisha vitu vyetu wenyewe au vitu ambavyo havijawahi fanywa na mtu mwingine yeyote. Wengi tunafanya haraka kuanzisha, ila badala ya kufika kwenye umiliki wa biashara (B) tunaishia kwenye kujiajiri katika biashara hizo (S).

SOMO LA KUMI NA MBILI @elimu_ya_utajiri



Unaposikia neno kazi yenye uhakika na malipo mazuri, jua maneno haya yanatolewa na mtu mwenye hofu ya kutokuwa na pesa. Yani mwenye mawazo ya ajira mara nyingi ndio yule ambae ana hofu labda kutokuwa na ajira kutamfanya awe na uchumi usioeleweka au huenda akawa maskini asipoajiriwa.  Linapokkuja suala la pesa watu wengi huona kama ajira ndo suluhisho kwa kuwa chochote atakachokifanya labda matumizi mabaya au mazuri mwisho wa mwezi lazima nyingine  itaingia tu. 
Wengi ya waajiriwa wanataka waajiriwe sehemu ambayo itakuwa inawapa huduma kama vile bima na mipango mizuri ya kupata kiinua mgongo pale wakiistaafu.
Jambo muhimu kwa watu hawa ni  kuondokana na  ile HOFU ya kutokuwa na pesa ifikapo mwisho wa mwezi na wanahitaji kuona uhakika huo ukiwa kwenye maandishi yaani MKATABA. Furaha yao kubwa ni hiyo kazi yenye uhakika, wao suala la uchumi usioeleweka hawataki kulisikia hata kwa bahati mbaya yaani eti ufike mwisho hajui kama atakuwa na hela au laaa? KWAO NI JAMBO GUMU KWELI KWELI.  Mara nyingi huwa na msemo unaopita vichwani mwao wakisema, “KAZI YAKO NITAIFANYA KAMA UNAVYOTAKA, ukiniahidi kunifanyia hiki na hiki" .

Wanahitaji kupunguziwa HOFU kwa kiwango fulani au kuondokana kabisa na hofu ya kutokuwa na pesa.... labda na SERIKALI au KAMPUNI  fulani. 
Pia hawakosei wanaposema hawahitaji kuzalisha pesa nyingi (kuwa MATAJIRI) kwa msemo wao wa “NAIPENDA KAZI YANGU”. Wengi hawaelewi kuwa hii inamaanisha kuwa wameweka kipaumbele uhakika wa kiasi fulani tu cha pesa mwisho wa mwezi kuliko KUZALISHA PESA kwenyewe. Waajiriwa wanaweza kuwa maraisi wa MAKAMPUNI fulani, mhudumu wa ofisi na wengine wengi tunaowafahamu. Wengi hawajali kazi gani wanazozifanya, wanachojali zaidi ni ule UHAKIKA tu wa KIMKATABA kila mwisho wa mwezi.
#KubadilikaKunaanzaNaKujuaWapiUlipo
#MatajiriWaKesho

SOMO LA KUMI NA MOJA @elimu_ya_utajiri



Hawa ni wale ambao wazungu wanasema “They want to be their own BOSS” yaani hawahitaji mtu yeyote awapangie suala la pesa wao ndio mabosi kwenye kazi yao, au wale ambao wanahitaji kufanya vitu kipekee yaani hajawahi fanya hivyo mtu mwingine yeyote au wale ambao wanataka kufanya kila kitu wenyewe. Hawa hawapendi kabisa kutegemea watu wengine katika suala pesa na wanataka kulipwa wakimaliza kufanya kazi zao.  Hawapendi mtu mwingine awaamulie kiasi cha pesa wanachotakiwa kukipata..hawapendi kuona mtu ambae hajafanya kazi kubwa kama wao anapata pesa zaidi yao. Pia wanafahamu wasipofanya kazi ya maana hawatakiwi kulipwa kiasi kikubwa yaani wanaamini ule msemo “wasipofanya kazi basi na wasile”. VIPI KUHUSU HOFU YA KUKOSA PESA?
Wakati waajiriwa wakijaribu kutoa hofu hiyo kwa kutafuta kazi yenye uhakika wa mshahara, hawa huamua kutoa hofu hiyo kwa kuingia kazini wenyewe na kupambana na kila hali. Katika kundi hili unawakuta wanataaluma mbalimbali ambao wametumia miaka mingi shuleni kama madaktari binafsi, wanasheria au mawakili binafsi n.k. Pia kundi hili linahusisha watu ambao hawajaenda shule kabisa au wale waliokimbia shule kama madalali wakubwa na wadogo, wauza maduka madogo madogo, wafanya usafi, mafundi bomba, seremala, mama ntilie wachungaji, wasusi, mafundi umeme, walimu wa Twisheni wanaofundisha vizuri sana, WASANII n.k. 
Nyimbo kubwa wanayoipenda ni ile ya “HAKUNA MTU ANAWEZA ZAIDI YANGU” au “NIMEFANYA KIVYANGU SIO KWA KUIGA”
Wengi ambao wapo katika kundi hili wanazifanya kazi zao vizuri sana yaani hawaamini kama kuna mwingine anaeweza kufanya kama wao na hii ndio maana tunawaajiri kutufanyia kazi zetu. 
Nani leo anataka kufanya wayaringi (wiring) nyumbani kwake akamchukua mtu ambae hayuko vizuri katika eneo hilo? Wote tutamtafuta yule fundi ambae alimfanyia vizuri jirani kwa sababu alifanya vizuri. Vipi kuhusu daktari wa meno? Daktari yeyote yule au aliyebobea katika eneo hilo? Na Vipi kuhusu wakili wa kukuendeshea kesi yako? N.k

Kwa watu wa kundi hili PESA sio muhimu sana kuhusu kazi yao, uhuru wa kufanya kazi, pesa ya kutopangiwa na kuheshimiwa kuwa  wako vizuri sana katika eneo lao walilobobea ndio mambo wanayoyapa kipaumbele.

SOMO LA KUMI @elimu_ya_utajiri





Wengi wetu kama sio wote tunawaza kuwa na Uhuru wa pesa siku moja ( kuimilikisha pesa) ila tatizo linakuja pale ambapo tumeamua kufanya fulani na ikaanza kwenye tofauti na tulitegemea, wengi wetu tutaamua kurudi sehemu ambayo tutapata uhakika wa kula na vitu vingine ( kutaka kupokea mshahara kila mwezi) tukisahau kwamba lengo sio kupata uhakika wa kula lengo ni kuja kuitumikisha pesa siku moja. Sasa kama biashara imeenda ndo inaamanisha uachane nayo uanze kuutegemea mshahara pekee?? kwanini usijaribu tena na tena mpaka pale itakapoenda vizuri? au jamani tumejua kuendesha baiskeli ghafla tu bila hata kudondoka dondoka mara mbili mara tatu?? kama tulivyopata mafunzo ya baiskeli ndo mafunzo ya kufanya biashara tuyachukulie hivyo.. Wote sisi ni binadamu ila linapokuja swala la pesa wengi tunaukimbikia ukweli tunaendeshwa na hisia au hofu zetu...ambazo hisia/hofu ndio zinatufanya tuamue kuganda katika eneo fulani(quadrant). Ukitaka kuwa katika eneo lingine lolote  unalolihitaji na kufanikiwa unatakiwa kuwa na maarifa ya yale yanayotolewa darasani. Pia inakupasa kufahamu utofauti mkubwa ambao unawafanya watu kujaribu kuwa katika maeneo tofauti ya yale waliyokuwa nayo sasa. (somo linalofuata). Ukijua utofauti huo utafanya maisha yako yote kuwa rahisi.
Cha kufahamu ni kwamba kila mtu anaweza kubadilika na kuwa katika eneo lolote analolihitaji... ila mabadiliko ya maeneo ya kuzalisha pesa ni tofauti na badiliko la kazi yaani kuamua kuacha kazi hii na kwenda kufanya kazi nyingine au kubadilisha taaluma ( mfano kutoka uhasibu kwenda kuwa mwalimu). Kubadilisha eneo (quadrant) kunahusisha na kubadilisha mtazamo  yaani jinsi unavyofikiri na jinsi unavyoifikiria dunia ya sasa. Badiliko la eneo ni rahisi kwa baadhi ya watu na ni ngumu kweli kwa baadhi ya watu wengine. Hii hutokana na kwamba kuna watu wako tayari kukubaliana na mabadiliko kuna wengine wao wako tayari kupingana na mabadiliko huku wakitetea mitazamo yao iliyopitwa na wakati. Badiliko la eneo ni suala ambalo ni la kujifunza maisha yako yote kwa kupata maarifa na uzoefu wa kila hatua unayokwenda sio jambo la siku moja au mbili. Unajifunza kutokana na mabadiliko ya wakati na dunia hii na kujua kutumia fursa.

SOMO LA TISA @elimu_ya_utajiri



Inawezekana kutengeneza pesa katika eneo lolote la JEDWALI LA MZUNGUKO WA PESA...pia inawezekana kutengeneza pesa kupitia maeneo yote pia, kumbuka kuzalisha pesa katika maeneo yote hiahusiaini na elimu inayopatikana darasani Bali inategemea utayari wa mtu, kujua madhaifu yako na sehemu gani uko vizuri. 
Utofauti uliopo kati yetu binadamu unatutofautisha katika maeneo ya kuzalisha pesa..mfano, kuna mwingine anapenda sana kuajiriwa ila kuna mwingine hataki hata hata kusikia habari za kuajiriwa...
kuna mtu anapenda kumiliki biashara fulani lakini hapendi kuiendesha mwenyewe... na mwingine anapenda kumiliki biashara hiyo na kuiendesha pia, kuna mwingine anapenda kuwekeza lakini mwingine anaogopa sana hasara (changamoto) ambazo ni sehemu ya kuwekeza...Usijali popote pale unaweza kuwa TAJIRI ni wewe tu. Mfano, mtu yeyote aliyeajiriwa anaweza ingiza pesa kupitia biashara ndogo ndogo au kubwa.

Kuwa katika eneo Fulani hakugarantii mafanikio yako..mfano, kujiajiri...wengi wamejiajiri katika biashara fulani au kazi fulani kama seremala mama Ntilie n.k lakini wangapi ni matajiri? tatizo ni sisi wenyewe. (tuna mengi ya kuyaongea hapa na ndio sababu iliyonituma mimi niwafikishe elimu hii watanzania wengi ambao TUMEAMUA KUJIAJIRI-kujiajiri tu sio suluhisho @elimu_ya_utajiri jumlisha kujiajiri ndio SULUHISHO)
Inachotakiwa kujua uko wapi na wapi unataka kufika, unahitajika kupata elimu ya eneo ulipo na eneo unalohitaji kufika siku moja. Ila bwana Robert Kiyosaki yeye anatuambia alichagua kuingiza pesa kupitia B na I kwa sababu aliona katika biashara kubwa na kuwekeza hakuna kodi na makato mengi. Kwahiyo kila siku alipambana kufika huko mpaka akafanikiwa...Anasema kwa kupambana kuzalisha pesa siku moja kupitia B na I kutakuwezesha kutengeneza pesa kwa haraka na pia kufanya pesa ikutumikie siku moja kama yeye alivyofanya.
JEDWALI LA MZUNGUKO WA PESA ni muhimu sana kwa kuwa linakuelezea na kukuonyesha njia mbalimbali ambazo pesa inazalishwa.  Pia anatuweka wazi njia ambazo tunaweza kuzalisha pesa bila kutoa jasho kubwa. Anazidi kutusisitizia kuwa kama tunahitaji kuzalisha pesa katika eneo fulani lazima tuwe na elimu jinsi mambo yanavyoenda katika eneo hilo.

SOMO LA NANE @elimu_ya_utajiri




Hiyo picha inayoonekana hapo juu ni kitu ambacho bwana Robert Kiyosaki anakiita CASHFLOW QUADRANTS tunaweza kuita JEDWALI LA MZUNGUKO WA PESA ...huu ni mgawanyo ambao unaonyesha maeneo mbalimbali ambapo tunazalisha pesa zetu.
E inawakilisha watu ambao wanaingiza pesa kupitia AJIRA (EMPLOYEE)
S inawakilisha watu ambao wanaingiza pesa kupitia biashara ndogo ndogo au kupitia kujiajiri kwao (SMALL BUSINESS au SELF EMPLOYED)
B inawakilisha watu wanaoingiza pesa kupitia biashara kubwa (BIG BUSINESS/BUSINESS OWNERS)
I inawakilisha wawekezaji (INVESTORS)- hapa pesa inazalisha pesa zaidi

Jedwali hili la mzunguko wa pesa bwana Robert Kiyosaki anajaribu kutuonyesha wapi tulipo na kutupa muongozo wa wapi inatakiwa tuwepo ili kufikia UTAJIRI WA UKWELI (utajiri ambao utafika hatua ambayo sio lazima kufanya kazi, kufanya au kutofanya ni maamuzi yako lakini unaishi vizuri na pesa zinazidi kuingia na kuongezeka). Anatuambia kuwa UTAJIRI huo unaweza kupatikana popote pale utakapokuwa katika mzunguko huo ila ukiwa na elimu ya  B na I itakusaidia kufikia malengo hayo kwa haraka zaidi
Kaa tayari nitakufikishia elimu hapahapa....elimu ambayo itakusaidia kutoka upande wa kushoto wa E na S kwenda upande wa kulia wa B na I. Cha kusisitizia tu kuwa elimu hii ni kwa wale tu ambao wako tayari kutoka kwenye kuitumikia pesa mpaka kwenye kuitumikisha pesa. Sio kazi rahisi kufikia ila ina thamani ya kuipambania elimu hii na kuitumia kama mwongozo katika maisha yako ya kila siku.....
#MjulisheNaMwingineKamaUnampenda
#MjulisheAnayeutakaUtajiri.

SOMO LA SABA @elimu_ya_utajiri






MATAJIRI HAWAITUMIKII PESA, WANAITUMIKISHA PESA
Hivi unajisikiaje kupanga mstari kusubiria pesa ya siku? au unajisikiaje pale tarehe uliyotegemea mshahara utoke na haukutoka? au unajisikiaje kuamka kila siku asubuhi na mapemaa kuwahi kibaruani ulipojiajiri na kurudi usiku nyumba nzima imelala? n.k

Endapo vitu kama hivi bado vinakutokea katika maisha yako...nikuambie tu ukweli kuwa unaitumikia pesa..ila nikupe moyo tu kuwa HAIMAANISHI kwamba hautaweza kamwe kuitumikisha pesa kama utaamua kubadilika leo hii ukawa na mtazamo wa kiTAJIRI.
Tunaambiana kila siku na tutaendelea kuambiana kuwa tujifunze kuitumikishe pesa sio kuitumikia milele. Muhimu kufahamu kwamba kusoma kuitumikisha pesa ni jambo ngumu linalohitaji utayari wa mtu binafsi na nia ya kuondokana na kizazi cha kimaskini. 
KWANINI NI NGUMU KUSOMA KUITUMIKISHA PESA?
Ni ngumu kwa sababu kuitumikisha pesa kunahusisha kufahamu changamoto mbalimbali zinazotokea katika kuwekeza na kukubali kuzikabili, uthubutu na msimamo wa kulisimamia jambo uliloliamua, utayari wa kupata funzo pale utakapofeli n.k. Wengi wetu hatuna vitu hivi zaidi tumejawa na mawazo hasi...badala ya kujengwa na changamoto sisi zinakuwa sababu ya kukata tamaa. Mfano, kama kuna mtu aliamua kuwekeza katika korosho msimu huu na matokeo yake msimu haujaenda vizuri kama ilivyozoeleka. Wengi walioanza kuwekeza katika zao hilo msimu huu ni wachache tu kati yao watakaoamua kuwekeza tena mwakani. WENGI WAMESHAAGANA NA ZAO HILO.....kifupi changamoto hazijawajenga...zimewakatisha TAMAA

KWANINI NI RAHISI KUSOMA KUITUMIKIA PESA? 
Kwanza kinachotufanya wengi tuamue kuitumikia pesa ni kutoka na HOFU. Wengi tunajiuliza:
Je, nikiweka pale pesa yangu..isipozalisha?? si ishakula kwangu
Nianze moja? nikishindwa kulipa kodi ya nyumba?
Kwa hiyo wengi tunaamua kwenda kuajiriwa  mahali Fulani tupate mshahara tupate uhakika wa kodi na mengine mengi huku tukijisahau kupambana kuitumikisha pesa siku moja. Lakini wengi tunaofanya maamuzi hayo ya kupata uhakika wa kodi tunaendelea kushangaa kwa nini matatizo ya pesa HAYAISHI.

Tunasahau kuwa tatizo ni kukosa elimu ya kuitumikisha pesa (elimu ya pesa @elimu_ya_utajiri). Chagua leo kuitumikia au kuitumikisha PESA.

Monday, March 18, 2019

SOMO LA SITA @elimu_ya_utajiri



PESA ni muhimu ila kilicho muhimu zaidi ni ELIMU YA PESA. PESA huwa na tabia ya kuja na kuondoka.....ila ukiwa na elimu ya pesa utajua jinsi gani pesa inavyokwenda, utaweza kuitawala na kutengeneza utajiri. Uwezo mzuri wa kufikiri kama ambao watu wengi waliosoma au wasiosoma wanao pekee hauwezi kukusaidia kuwa TAJIRI.....hii ni kwa sababu wengi tumeenda shule lakini hatujafundishwa kuhusu kuitumikisha pesa tumefundisha kuitumikia pesa.
Elimu ya pesa itakuongoza wewe pamoja na kizazi chako kuwa MATAJIRI na kufanikiwa mazingira yoyote yale, kama uliweza kutengeneza pesa kipindi cha mh. Kikwete pia utaweza tengeneza pesa kipindi cha mh. Rais Magufuli na katika hali nyingine yoyote ile inayokuja mbeleni. Elimu ya pesa (@elimu_ya_utajiri) ipo kukupa muongozo wa kukufanya upate utajiri.
Mwalimu mzuri zaidi kuliko wote ni maisha, kuna muda yanatukaba yaani pesa ukiitafuta haipatikani, ukipata kazi mshahara unaonekana mdogo au unapata kazi inaonekana ni ngumu. Unachotakiwa ni kujua kuwa ..hayo ni mafundisho ya maisha yanayokutaka uamke kutoka kwenye usingizini. 
Kuna baadhi watakubali tu wacha maisha yaendelee kuwakaba kwa kuona hawana cha kufanya....ila wengi wetu tutapata hasira tutaamua  kupambana, lakini badala ya kupambana na maisha tutapambana na maBOSS wetu tukidai pesa tunazolipwa ni ndogo au tutapambana na kazi zetu tukidai kazi hii hailipi kabisa bora kazi fulani, na wengine huenda mbali zaidi mpaka kupambana na mume au mke. Tunasahau kwamba maisha ndo tunayotakiwa kupambana nayo.

CHUKUA SOMO HILI....Inatupasa kujilaumu sisi wenyewe kuliko kuwalaumu wengine kutokana na matatizo yetu. Kama unahisi tatizo ni mtu fulani basi fanya hima kumbadilisha ili maisha yako yabadilike, ila kama utachukulia kuwa tatizo ni lako ni rahisi kujibadilisha kuliko kumbadilisha mwingine. TUJIBADILISHE
Tunatakiwa wote kupata somo hili kwa kuwa ndilo ambalo litatupelekea kuwa wastaarabu na kuupata utajiri tunaoutaka..... la sivyo tutaishia kulaumu kazi zetu, mshahara mdogo au mabosi, huku tukiendelea kujipa matumaini kuwa kuna siku moja isiyokuwa na jina tutapata zari la pesa litakalomaliza matatizo yetu yote. 
#MjulisheNaMwingine
#MatajiriWaUkweli
#TunaMengiYaKufundishana

SOMO LA TANO @elimu_ya_utajiri



MATAJIRI WANAFANYAJE? Unataka kuwa TAJIRI halafu unajiuliza matajiri wanafanyaje? sio kitu kipya kukisikia..siri kubwa ya Matajiri ni kuelekeza nguvu zao zaidi katika rasilimali (assets) ambazo zinawaingizia pesa sio katika vitu vingine ambavyo vinakula pesa (liabilities). Rasilimali kwa mujibu wa @elimu_ya_utajiri ni kitu chochote ambacho kinakuingizia pesa mfukoni mwako na hivyo vitu vingine (liabilities) ndo vitu ambavyo vinatoa pesa mfukoni mwako. Ambao hawautaki UTAJIRI wanakosea wapi? wengi wetu tukipata vijisenti kidogo tutakachokiwaza ni kununua TV nzuri zaidi, kununua king'amuzi kizuri zaidi, kubadilisha ile deki ya zamani, kununua gari au pikipiki na mengine mengi ambayo hayatuingizii pesa zaidi ya kupunguza pesa zilizopo mfukoni .....Yatupasa kubadilika na kuanza kuwaza vitu ambavyo vitatuingizia pesa kupitia hizihizi pesa ndogo tulizozipata.... @elimu_ya_utajiri inakutaka kabla hujaamua kununua kitu unachotaka kununua....Fikiria ishu utakayoifanya ikakuingizia pesa ili hi

Face the challenge